Haya ni “MAISHA YA MJINI” yenye wingi wa misururu ya visa na mikasaa…Ndilo VUMBA hilo la maisha! Au ni SHOMBO? Litatakaswa na nani? JE, TUFANYEJE? Safari inang’oa nanga sasa. Safari yenye pandashuka ya maisha. Haya mjukuu wangu! keti kitako, ubwabwa koponi, kitabu mkononi!
Hassan Mwana wa Ali ni mhariri wa habari za michezo katika shirika la Standard. Licha ya kutangaza mpira na vipindi vya michezo, yeye ndiye nahodha wa kipindi cha NURU YA LUGHA, Radio Maisha kila siku za Jumamosi, saa moja hadi tano asubuhi. Aidha, huchangia makala mbalimbali ya elimu, siasa, dini na kadhalika katika gazeti la Taifa Leo na jarida la Nairobian, na ni mshereheshaji wa sherehe mbalimbali. Vilevile, ameandika kazi kadha wa kadha za Fasihi ikiwemo, riwaya ya PICHA YA KARNE iliyoshinda tuzo ya Jomo Kenyatta mwaka 2019. Hadithi zake zinapatikana kwenye mikusanyiko kadha wa kadha kama vile GITAA, SINA ZAIDI, MASKINI MILIONEA, KUNANI MAREKANI, UTASHI WA DOLA, KITI CHA SIMANZI na kadhalika.
Amewahi kushinda tuzo ya mtangazaji bora wa soka nchini Kenya mwaka 2011; mwanahabari bora wa michezo redioni mwaka 2021/2022 na tuzo za wanahabari nchini, AJEA. Pia ametuzwa mara kadhaa kwenye tuzo za kila mwaka za KUMIKUMI ambazo huandaliwa WASTA. Fauka ya haya, amechangia katika ukusanyaji wa maneno kwenye baadhi ya KAMUSI.